Vipengele vya fasihi vinavyojenga taswira ya mwanamke katika vitabu teule vya Biblia takatifu
Abstract/ Overview
Lugha ni chombo cha kipekee kinachofinyangwa kuwasilisha taswira ya masuala changamano katika jamii. Lugha inapofinyangwa huzua fasihi, ambayo ni kioo cha jamii. Biblia Takatifu ni kitabu mojawapo kikongwe cha fasihi ambacho mafunzo yake hurejelewa na zaidi ya watu bilioni 2.4. Katika Biblia Takatifu, kitabu cha Mwanzo 1:26-27, lugha inatuchorea taswira kuhusu hadhi sawa ya mwanamke na mwanamume kulingana na mpango asili wa Mungu. Hata hivyo, katika hiyo hiyo Biblia Takatifu tunakumbana na taswira changamano kumhusu mwanamke. Utafiti huu ulichanganua vipengele vya fasihi vinavyojenga taswira ya mwanamke katika vitabu teule vya Biblia Takatifu. Madhumuni mahsusi ni: kubainisha maumbo ya fasihi yanayojenga taswira ya mwanamke katika Biblia Takatifu, kupambanua mitindo ya lugha inayojitokeza katika maumbo ya fasihi yanayojenga taswira ya mwanamke katika Biblia Takatifu na kuchanganua maudhui yanayojitokeza katika maumbo na mitindo ya lugha inayojenga taswira ya mwanamke katika vitabu teule vya Biblia Takatifu. Utafiti ulizingatia kiunzi cha nadharia chenye mihimili kutoka nadharia tatu; nadharia ya Umaumbo iliyoasisiwa na Shlovsky (1904) na kuendelezwa na Maryanne (1999); Umuundo mpya iliyoasisiwa na Derrida (1972) na kuendelezwa na Crick (2016) na Ufeministi huru kwa mujibu wa Wamitila (2003) iliyoasisiwa na Bouchier (1983). Mihimili ya nadharia ya umaumbo kuwa kazi yoyote katika fasihi ina sifa teule kisanii zinazomwongoza anayetafiti. Pili, kwa sababu fasihi inajumlisha lugha, lugha ni mhimili katika sayansi ya fasihi. Tatu, fasihi haiwezi kutengwa na jinsi inavyowasilishwa kwani umbo la kazi huirembesha na pia ni sehemu ya yaliyomo. Mihimili ya nadharia ya Umuundo mpya iliyotumiwa n maana huumbwa kwenye lugha na lugha ni mhimili mkuu katika kuchanganua maswala katika jamii. Mhimili wa nadharia ya ufeministi huru uliotumiwa ni ule unaomuongoza mhakiki kushambulia yaliyoandikwa na namna wanavyowasilisha wahusika wanawake. Utafiti ulizingatia muundo wa kiuchanganuzi. Idadi lengwa ilikuwa vitabu 66 vya Biblia Takatifu. Kwa kuzingatia madhumuni ya utafiti usampulishaji dhamirifu ulifanywa kufikia kiwango ambacho hakuna data nyingine mpya ilipatikana. Vitabu 12 vilisampuliwa; Mwanzo, Waamuzi, Ruthu, Wafalme 1 na 11, Esta, Methali, Wimbo ulio Bora na Luka Mtakatifu, Matayo, Samweli I na II. Orodhahakiki ilitumiwa kudondoa data ya maumbo, mitindo na maudhui yanayojenga taswira ya mwanamke katika Biblia Takatifu. Data ilipangwa na kuwasilishwa kimaelezo. Matokeo yalibaisha kuwa maumbo ya fasihi yanayojenga taswira ya mwanamke katika Biblia Takatifu huwasilishwa kwa mitindo teule ya lugha inayodhihirisha maudhui yanayojenga taswira hasi au chanya kumhusu mwanamke. Utafiti unatarajiwa kuwafahamisha wanajamii kuwa fasihi ni namna ya kipekee ya kutumia lugha kujenga taswira ya maswala changamano katika jamii.